POLISI WAMUUA MSHUKIWA WA MAUAJI UFARANSA
By Maganga Media - Mar 22, 2012
Mohamed Merah |
Mshukiwa wa mauji ya watu wanne katika shule ya Kiyahudi mjini Toulouse Kusini mwa Ufaransa siku ya Jumatatu Mohammed Merah ameuawa katika makabiliano na polisi katika makaazi yake. Polisi walivamia nyumba ya mshukiwa huyu baada ya harakati zao za kumtaka Merah mwenye umri wa miaka 23 raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria kujisalimisha kutofua dafu kwa saa 32.Waziri wa mambo ya ndani Claude Gueant amesema mshukiwa huyo alikuwa amejificha bafuni na alipowaona polisi alianza kuwafwatulia risasi kabla ya kuruka dirishani na alipatikana akiwa ameuawa baada ya kuanguka chini.
Katika makabiliano hayo, polisi watatu walijeruhiwa mmoja akipata majeraha mabaya mguuni na kukimbizwa hospitalini kupata matibabu. Mshukiwa huyo alikiri kuwa mwanamgambo wa Al-Qaeda aliyepata mafunzo kutoka Pakistan na Afganistan alituhumiwa pia kuwaua wanajeshi watatu Kusini mwa nchi hiyo wiki mbili zilizopita,mauji ambayo alisema alitekeleza kutokana na majeshi ya Ufaransa kuwa nchini Afganistan. Polisi waliamua kuvamia makaazi yake baada ya kupoteza mawasiliano naye usiku kucha na walitumia milipuko kadhaa kumtisha ili ajisalimishe kwao bila mafanikio.
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkzoy amesema kila juhudi zilifanywa kumkamata Merah akiwa mzima ili afunguliwe mashtaka na kuonya kuwa serikali yake inaendelea kufanya uchunguzi zaidi ya ugaidi hasa kwa wale wanotumia mitandao na wanaosafiri katika nchi za kigeni kupata mafunzo ya kigaidi. Kiongozi wa mashtaka Francois Molins amesema Merah apigwa risasi kichwani wakati akiruka dirishani,na pia alipiga picha na kuchukua video alivyotekeleza mauji ya watoto watatu na mwalimu wao katika shule ya Kiyahudi siku ya Jumapili.
Kuuawa kwa mshukiwa huyo kunatamatisha oparesheni hiyo ya siku mbili ya kujaribu kumkamata baada ya kutekeleza mauji ya watu saba.
CHANZO: RFI
Maganga Media
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII