ARUMERU; KAMPENI ZA MWISHONI
By Maganga Media - Mar 28, 2012
Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arumeru mashariki mchuano mkali wa maneno na vijembe umeendelea kupamba moto katika kuhakikisha kila upande unachukua ushindi wa jimbo hilo. Ingawa vyama vinane vimesimamisha wagombea, hadi sasa Chadema na CCM ndiwo wanaonekana kuchuana katika harakati za kunyakua jimbo hilo lililoachwa wazi na Jeremiah Sumari (CCM) aliyefariki Januari mwaka huu. Vyama vingine vinavyoonekana kama wasindikizaji ni pamoja na TLP, Sau, AFP, UPDP, DP na NRA, huku vingine vikishindwa kufanya mikutano ya kampeni.
Miongoni mwa yaliyojili huko ni Kauli ya Dr Wilbroad Slaa akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguni. Amewakumbusha kuwa uchaguzi huo umeangukia siku mbaya kwani ni siku ya wajinga duniani tarehe 1 mwezi wa April. Hivyo amewataka wapuuze taarifa zozote zinazoweza kutolewa kuwa siku hiyo hakuna uchaguzi na uongo mwingine ufananao na huo.
Miongoni na vijembe vilivyotawala jana ni pamoja na kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. Sugu dhidi ya ombi la makada wa CCM la kutaka mgombea wao, Sioi Sumari, apewe ubunge ili kumfuta machozi kutokana na kufiwa na baba yake, Jeremiah Sumari ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki. Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nshapu Kata ya Nkoaranga, Sugu alikejeli ombi hilo na kusema kuwa ubunge hauwezi kumfuta mtu machozi.
Alisema: “Kama ingekuwa hivyo basi, Rais wa Tanzania leo angekuwa Madaraka Nyerere au Makongoro, maana nao ni wafiwa, tena baba yao tunamheshimu kwa kuwa alikuwa Baba wa Taifa.” Sugu alirusha kijembe hicho kwa lengo la kumjibu Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, ambaye amekuwa akimwombea kura Sioi kwa kuwataka wananchi wamchague ili wamfute machozi kwa sababu amefiwa na baba yake.
Mbowe abeza kampeni za matusi
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amewataka wanachama wa chama hicho kutojibizana na wanachama wa CCM ambao kwa sasa wanatumia majukwaa ya kampeni kuwatukana viongozi wa CHADEMA na mgombea ubunge wa chama hicho, Joshua Nassari. Badala yake amewataka wawaombee ili waache matusi na wasichakachue kura siku ya uchaguzi kwa kile alichoeleza kuwa mpaka sasa kwa tathmini waliyofanya mgombea wa chama hicho atashinda huku CCM ikiangalia.
Mbowe aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa chama hicho kwenye mikutano mbalimbali kwenye kata za Leguruki, Nkoaranga, Akheri, Nkoarisambu, Songoro na Mbuguni. Alisema kuwa ni vema wananchi wa Arumeru Mashariki wakaishi kwa amani lakini si kwa woga wakielewa kuwa uchaguzi utapita lakini wao watabaki. “CCM wameamua kuendesha siasa za matusi, wanatukana viongozi wakuu wa CHADEMA, wanatukana wabunge wetu pamoja na mgombea wetu Nassari, nyie msijibizane nao mnachotakiwa kufanya ni kuwaombea kwenye mikutano yao waache matusi, tuwaombee siku ya kupiga kura wasichakachue huku tukiendelea kuwashawishi wampigie kura mgombea wetu ili kuongeza asilimia ya ushindi,” alisema Mbowe.
Kwa upande wake mgombea wa CHADEMA, Nassari alikemea wale wanaofananisha uchaguzi huo na mchezo wa maigizo au mpira wa miguu (soka) kwa kile alichoeleza kuwa uchaguzi huo ni muhimu sana kwani ndiyo unaoenda kuamua mustakabali wa wananchi wa Arumeru Mashariki ambao kwa kipindi kirefu wamekosa mwakilishi makini wa kushughulikia kero zao kwenye vikao mbalimbali vya maamuzi. Alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni 141 za mfuko wa maendeleo ya jimbo (CDF) ambazo zilitolewa kwa ajili ya jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitatu cha kuanzia 2010 mpaka 2012 hazijulikani zimefanya nini wakati kimsingi zilipaswa kutumika kutatua matatizo ya jimbo hilo kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu na maji.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII