HABARI MPYA LEO  

By Maganga Media - Feb 14, 2012

Tujivunie nini matokeo ya kidato cha nne 2011?
Tuesday, 14 February 2012 15:12
WIKI iliyopita Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika Oktoba mwaka jana.
kiwango cha ufaulu mwaka 2011 kimeongezeka kwa asilimia 2.63. Kwa mujibu wa takwimu za baraza, kiwango cha ufaulu mwaka huu kimefikia asilimia 53.59  kutoka asilimia 50.74 ya mwaka 2010.

Aidha, tofauti na matokeo yaliyopita, safari hii wavulana wameibuka vinara wa ufaulu kwa kupata asilimia 57.51 dhidi ya asilimia 48.25  ya wasichana walioongoza katika mtihani wa mwaka 2010.



Watu wengi hususan wadau wa elimu walikuwa na shauku kubwa kujua matokeo ya  mwaka 2011, hasa wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya mwaka 2010 yaliyoshuhudia idadi kubwa ya wahitimu  wakifeli mtihani huo.
Hata hivyo, swali muhimu ni je, kuna cha kujivunia kutokana na matokeo haya?

Mwanaharakati wa masuala ya elimu, Daudi Solomon anasema japo zaidi ya nusu ya wanafunzi (asilimia 53.59) wamefaulu kwa takwimu za baraza, bado ongezeko la kiwango cha ufaulu kwa asilimia 2.63, siyo suala la kujivunia.
Kwa upande wake, haoni kama matokeo hayo yana ahueni yoyote, kwani kiwango hicho cha ufaulu kinachoelezwa kukua kinajumuisha pia wanafunzi waliopata daraja la nne ambalo kwa taratibu za baraza wanahesabika wamefaulu.
Kwa mujibu wa  takwimu zilizotolewa na baraza, ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa unaonyesha, jumla ya watahiniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo, wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.

Kwa sura hiyo, wanafunzi wanaoelezwa ‘kufaulu’kwa kiwango cha daraja la nne ni 146,639 ambao ni sawa na asilimia 43.60.

“Kwa hiyo katika ule ufaulu  wa asilimia 53 unaosemwa umeongezeka, kumbe asilimia zaidi ya 40 ni ya hao wanafunzi wa daraja la nne. Hayo siyo mafanikio ya kuringia, ingekuwa bora kama waliopata daraja la kwanza hadi la tatu wangekuwa wengi,’’anaeleza Solomon.

Mkuu wa asasi ya Twaweza, Rakesh Rajani anayesema: “Kwanza maana halisi ya mtu aliyefaulu, ni yule aliyepata kuanzia daraja la kwanza mpaka la tatu, chini ya hapo amefeli.“Kwa maana hiyo, basi waliofaulu huu mtihani ni asilimia 9.98 ya wahitimu wote waliofanya mtihani huu, kwa sababu hawa ndio waliofaulu kwa daraja hilo la kwanza mpaka la tatu.’’

Kitakwimu ni kweli kuwa kiwango cha ufaulu safari hii kimeongezeka ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2010.Hata hivyo,  kiuhalisia matokeo haya yanaakisi nini kwa upande wa wahitimu?

Bila shaka kati ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo, ni wahitimu 33,577 wanaoweza kuendelea na kidato cha tano iwe kwa kuchaguliwa katika shule za Serikali au kujiunga na shule binafsi.

Nini hatima ya jeshi la wahitimu 146,639 waliopata daraja la nne na 156,089 waliopata daraja sifuri? Hawa wanakwenda kufanya nini mtaani?, Je, jamii itegemee nini kutoka kwao?

Mara kwa mara wadau wa elimu wamekuwa wakiukosoa mfumo rasmi wa elimu nchini kwa kushindwa kuwaandaa wahitimu wa madaraja mbalimbali ya elimu, kumudu changamoto za kimazingira na zile za maisha.
Wanasema mfumo huo umeegema zaidi katika kuwachuja wanafunzi kupitia mitihani, huku ukiwaacha bila msaada wowote wanaofeli katika madaraja hayo.

Kimsingi,  mfumo huo   hauwaandai wahitimu kujitegemea kimaisha kwa kuwa mitalaa inayotumika ni ile ya elimu ya jumla na iliyojaa nadharia, badala ya kutoa msisitizo katika elimu ya ufundi na stadi za maisha.

Ni kwa sababu ya upungufu huu wa kimfumo, mara kwa mara kumekuwa ni wito, tena kutoka kwa viongozi,  wanaowataka wanafunzi wanaofeli darasa la saba au kidato cha nne, kwenda kusomea elimu ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na  Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Kama mfumo wetu ungekuwa unajitosheleza, kusingekuwa na haja ya wahitimu wa elimu rasmi kwenda kusoma katika vyuo vya ufundi,kwani mafunzo hayo wangeyapata katika shule za kawaida.
Aidha, ukitoa uwezo wa kujitegemea, je, wahitimu wa sasa wa kidato cha nne wakiwamo hao wanaoelezwa kufaulu, wanaweza kuajiriwa na kufanya kazi kwa ufanisi?

Waliosoma enzi za mfumo wa elimu wa kikoloni, pamoja na upungufu wake, wanakiri namna wahitimu hata wa madaraja ya chini katika mfumo huo walivyoweza kufanya kazi katika kiwango cha kuridhisha.
Uzoefu wa Kenya

Kenya ipo mbioni kufanya mabadiliko ya kihistoria katika mfumo wake wa elimu. Kwa mfano, hivi sasa nchi hiyo siyo tu  inatarajia kubadili mfumo wa elimu wa 8-4-4  na kuwa 2-6-6-3, lakini mpango uliopo ni kuwa na shule za  zitakazokuwa zikitoa  aina nne za mafunzo ambazo wanafunzi watapewa uhuru wa kuyachagua.
Kwa mujibu wa ripoti ya timu iliyoandaa mabadiliko hayo, aina hizo nne za mafunzo inajumuisha elimu ya jumla, elimu ya ufundi stadi, elimu ya vipaji maalumu na

Ripoti inasema timu ya wataalamu ilipendekeza kuwapo kwa aina hizo za elimu,  kwa kuwa hata watakaoshindwa kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari au vyuo vikuu, bado watakuwa na fursa ya kujiendeleza katika fani walizosomea.

Bado kwa Tanzania, wahitimu wa mfumo wa sasa wa elimu ya msingi na sekondari ,  wanakosa maarifa na  stadi za kumudu mazingira yanayowazunguka. Wengi wao hupotea mitaani baada ya kufeli.
Hali ya shule za umma

Kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2010, shule za umma hasa zile za  kata zimeendelea kufanya vibaya.
Sababu za kufanya vibaya kwa shule hizo ni nyingi zikiwamo kubwa  za  uhaba wa walimu, vifaa vya kujifunzia kama vitabu, ukosefu wa maabara na maktaba.
Ni kwa sababu hii, matokeo katika shule nyingi za kata zinaonyesha wahitimu wengi wamepata daraja sifuri na wachache daraja la nne.

Kwa mfano, katika Shule ya Sekondari Maneromango ya mkoani Pwani iliyokuwa na watahiniwa 108, wahitimu 102  wamepata daraja sifuri na  sita wamepata daraja la nne.  Shule nyingine ni Kibuta pia ya mkoani humo ambayo wahitimu wake 80 kati ya 86 waliofanya mtihani, wamepata daraja sifuri.
Kibaya zaidi, bado Serikali haijazitazama shule hizi kwa jicho la huruma.Pamoja na ongezeko la bajeti ya elimu hasa katika miaka ya karibuni , inasikitisha ile  ahadi ya  Serikali kuzipa shule ruzuku za  wanafunzi ili kuboresha taaluma shuleni, imeshindwa kutekelezeka kwa ukamilifu.

Kwa mfano, utafiti  wa mwaka 2011 kuhusu ruzuku za wanafunzi uliofanywa kwa pamoja na asasi za kiraia za HakiElimu, Twaweza na Policy Forum,  unaonyesha ruzuku hizo hazitolewi kwa walengwa na hata zikitolewa,hazifiki kwa wakati au zinatolewa chini ya kiwango ambacho ni Sh 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Serikali, mpango wa ruzuku kwa wanafunzi shuleni ulianzishwa ili pamoja na mambo mengine ulenge kuinua taaluma kwa kuhakikisha rasilimali muhimu kama vifaa vya kujifunzia zinapatikana shuleni.
Source:
http://www.mwananchi.co.tz/makala/-/20223-tujivunie-nini-matokeo-ya-kidato-cha-nne-2011

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII