HABARI MPYA LEO  

Serengeti Boys wapimwa umri!

By Unknown - Jul 17, 2012

Release No. 121

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Julai 17, 2012

Wachezaji 17 wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) wamefanyiwa vipimo vya kubaini umri wao halisi (MRI Tests) kwenye hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Upimaji huo ulifanyika Julai 14 mwaka huu chini ya usimamizi wa mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk. James Sekajugo kutoka Uganda na Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Dk. Sylvester Faya.

Dk. Sekajugo alisema vipimo hivyo vya Magnetic Resonance Imaging (MRI) vinafanya kutokana na maelekezo ya CAF kwa nchi zote ambazo zitashiriki mashindano ya U17 ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Morocco ili kubaini umri halisi wa wachezaji hao.

Amesema vipimo vya MRI havina madhara kama ilivyo kwa X-ray ambapo vyenyewe vinachunguza uimara wa mifupa ili kubaini umri halisi wa mchezaji, na uwezo wake ni kubaini watu walio chini ya umri wa miaka 17.

CAF imeamua vipimo hivyo vifanyike kabla ya wachezaji kuingia kwenye mashindano kwani Afrika inakabiliwa na tatizo sugu la kudanganya umri wa wachezaji.

“Naipongeza TFF kwa kuhakikisha upimaji unafanyika kama ilivyoagizwa na CAF. Wakati mwingine si udanganyifu, unajua katika Afrika hakuna utaratibu wa watoto kuandikishwa wanapozaliwa. Hivyo inawezekana kabisa mtoto au mzazi wake hakumbuki au hajui tarahe aliyozaliwa,” amesema Dk. Sekajugo.

Amesema uamuzi wa CAF kufanya vipimo vya MRI kabla ya wachezaji kuanza mashindano umelenga kuhakikisha wachezaji wanaoshinda wana umri sahihi, badala ya vipimo hivyo kufanyika wakati wa fainali.

“Mwaka 2005 CAF iliamua kufanya vipimo hivyo miezi miwili kabla ya kuanza michuano ya fainali. Kuna timu moja ilikutwa wachezaji wake wote wamezidi umri, hivyo ikabidi waunde timu mpya,” amesema Dk. Sekajugo na kuongeza kuwa matokeo ya vipimo vya wachezaji wa Serengeti Boys vitatumwa baada ya wiki mbili.

Naye Dk. Faya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF amesema wachezaji 10 waliobaki watafanyiwa vipimo hivyo baadaye kabla ya mechi ya michuano hiyo CAF dhidi ya Kenya itakayochezwa Septemba mwaka huu.

Wachezaji tisa wako nchini Burundi kwenye michuano ya Rolling Stone Multipurpose Acre Foundation wakati mmoja (Dickson Ambundo) amekwenda Ujerumani na timu ya TASC ya Mwanza.

Walioko Burundi ni Hamad Juma, Mgaya Jaffar, Ismail Gambo, Mohamed Hussein, Hussein Ibrahim, Mudathir Abbas, Farid Shah, Joseph Lubasha na Kelvin Friday.

Dk. Faya amesema vipimo vya MRI kupanywa mapema ni vizuri kwa sababu tatizo la udanganyifu wa umri lipo, lakini pia litaisaidia TFF kwani inatumia gharama kubwa kuandaa timu, hivyo ni vizuri ikaandaa timu ya wachezaji wenye umri sahihi badala ya waliodanganya umri ambao hawataruhusiwa kushiriki mashindano.

Mwaka 2005 Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali za Afrika zilizofanyika Banjul, Gambia lakini ilinyang’anywa nafasi hiyo baada ya kubainika kuwa baadhi ya wachezaji wake walikuwa wamezidi umri wa miaka 17.

Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII