HABARI MPYA LEO  

Mnyika ahojiwa kuhusu mauaji ya Singida

By Unknown - Jul 19, 2012

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
MBUNGE wa Ubungo (Chadema), John Mnyika jana alihojiwa na polisi kutokana na vurugu zilizosababisha kifo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kata ya Ndago, wilayani Iramba, Yohana Mpinga (30).Mnyika ni mmoja wa viongozi wa Chadema ambao walihutubia mkutano huo uliofanyika katika Jimbo la Singida Magharibi.Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Robert Manumba alieleza nia ya jeshi hilo kutaka kumhoji Mnyika kuhusu tukio hilo, lakini hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hili akishauri aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.

Mnyika aliyekwenda Singida kuitikia wito wa polisi, alihojiwa na kikosi maalumu cha maofisa wa jeshi hilo kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam, ambao wako mkoani humo kuchunguza matukio ya vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha kifo cha kada huyo wa CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida jana, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kuwa, Mnyika alifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida jana saa 7.45 mchana kuitikia wito  uliotumwa kupitia Ofisi za Bunge.

Makene alimnukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa akisema, Mnyika anapaswa kuhojiwa na kikosi maalumu cha maofisa wa Polisi kutoka Dar es Salaam ambacho kwa wakati huo, kilikuwa Ndago kufanya upelelezi wa kitaalamu zaidi kuhusiana na mauaji ya Yohana.
“Kutokana na kauli hiyo, hivi sasa Mbunge Mnyika amepumzika hadi hapo saa kumi jioni, atakapohojiwa na hicho kikosi maalumu, anahojiwa kuhusu nini, hiyo ni siri hakuna anayefahamu,” alisema Makene.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyika alisema akiwa katika Ofisi ya RPC Sinzumwa alihoji iwapo alitakiwa kuhojiwa kama mtuhumiwa au shahidi.“Jibu la RPC ni kwamba ni mahojiano ni ya kawaida tu, nilihoji sababu Mwita (Mwikwabe) aliambiwa kwamba ni mahojiano ya kawaida, lakini baadaye aliwekwa ndani na kupandishwa kizimbani,” alisema Mnyika.
 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII