Mahakama kuu yakubali kuchunguza umri wa Lulu
By Maganga Media - Jun 12, 2012

Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa Mahakama Kuu Mei 15 na mmoja wa mawakili wake, Peter Kibatala walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo. Mawakili wa mshtakiwa huyo walidai kuwa mshtakiwa huyo bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyosomeka na kwamba na maana hiyo anapaswa kushtakiwa katika Mahakama ya Watoto (Juvenile Court).
Akitoa uamuzi wa maombi hayo jana Jaji Dk Fauzi Twaib alitengua na kutupilia mbali uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi kukataa kuwa haina uwezo wa kushughulikia maombi hayo, akisema kuwa mahakama hiyo ilikosea. Jaji Dk, Twaib alielezea kushangazwa kwake na Mahakama ya Kisutu kukataa maombi hayo akisema kuwa ilikosea kwa kuwa ina mamlaka ya kuyashughulikia.
Kutokana na mazingira hayo Jaji Dk Twaib alisema kuwa kuna njia mbili ambazo moja ni kuwasilisha upya maombi hayo mahakamani hapo na ya pili ni mahakama hiyo kutumia mamlaka yake chini ya Kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi kujiridhisha usahihi wa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu. Alisema kulingana na unyeti wa kesi hiyo Mahakama Kuu kwa kutumia mamlaka yake na kwa kuzingatia kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi imeamua kufanya uchunguzi huo yenyewe.
Aliongeza kuwa kwa sababu hizo ameamua kutumia kifungu cha 44(1) cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, ili Mahakama hiyo iweze kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo kama ilivyoombwa na waombaji.
Sambamba na uamuzi huo Jaji Twaib aliamuru upande wa waombaji kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo na nyaraka za ushahidi wa umri wa mteja wao kesho. Pia aliauagiza upande wa wajibu maombi (Jamhuri) kuwasilisha mahakamani ushahidi wowote kuunga mkono msimamo wake Juni 20, 2012 na Juni 22, 2012 muombaji awasilishe majibu ya ufafanuzi (Rejoinder) na akaamuru maombi hayo kusikilizwa Juni 25, 2012.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII