HABARI MPYA LEO  

ECOWAS yasimamisha Uanachama wa Mali

By Maganga Media - Mar 28, 2012

Akihutubia waandishi wa habari baada ya mkutano huo Rais wa Ivory Coast, alisema Amadou Toumani Toure bado yuko hai na yuko katika hali njema . Kiongozi huyu wa Ivory aliongezea kuwa alizungumza na Toure saa chache kabla ya mkutano wao kuanza. Na kwa wale waliohusika na kumwangusha madarakani rais wa Mali, ECOWAS imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kusitisha uanachama wao katika chombo hiki, kulaani mapinduzi hayo ya kijeshi na kutishia kuiwekea vikwazo nchi hiyo iwapo viongozi wapya wa kijeshi hawatarejesha utawala wa katiba.

Nae mwenyekiti mpya wa Tume ya ECOWAS, Kadre Desire Ouedraogo, ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa na kumchagua Rais Blaise Compaore wa Burkina Faso kuwa msuluhishi wao. "Mkutano huu unaidhinisha kuyapa uwezo majeshi ya akiba ya ECOWAS kujiandaa kwa kila tukio. Endapo kutatokea kutoheshimu maamuzi ya CNRDR, mkutano unawaagiza wanachama wote kuweka mara moja vikwazo vya usafiri na kidiplomasia na fedha dhidi ya watawala hao wa kijeshi na marafiki zao,” Desire-Ouedraogo alitangaza "

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara anatarajiwa kuongoza ujumbe wa viongozi sita wa nchi za Afrika Magharibi kwenda Mali kukutana na viongozi wa kijeshi. Rais Ouattara pia amesema viongozi hao wa kijeshi wamekwisha taarifiwa kuhusu msimamo wa ECOWAS. Rais wa Ivory Coast amesema kwa wakati huu, mazungumzo yanahitajika zaidi katika kutatua mgogoro wa kikatiba nchini Mali, lakini amesema hawatasita kutumia njia nyingine zote mbadala iwapo hii itashindikana.

Kikundi cha viongozi wa kijeshi wa kanda hiyo pia nao wamepanga kwenda Bamako kuwashauri viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini pia kuweka wazi namna  ECOWAS itakavyosaidia kukabiliana na mashambulio ya waasi kaskazini mwa nchi ya Mali.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII