Kafulila ataka Mbunge aliyekamatwa kwa rushwa avuliwe ubunge
By Maganga Media - Jun 5, 2012
TAMKO LA NDUGU DAVID KAFULILA KUHUSU MBUNGE WA JIMBO LA BAHI KUKAMATWA NA TAKUKURU KWA RUSHWA.
JUNE 03, 2012
Ningependa kuwakumbusha wana habari kuwa nimepata kuzungumza Bungeni mwaka jana 2011 kuhusu tabia ovu kwa baadhi ya wabunge kuomba rushwa watumishi wa serikali katika mchakato wa kusimamia serikali. Ilikuwa ni Bunge la mwezi June, tarehe 13, 2011 wakati nikichangia hoja ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Hapa nilitoa taarifa iliyowahusu wabunge watatu akiwemo huyu anayeshikiliwa na vyombo vya dola sasa, Ndugu Omary Badwel. Kwakuwa hakuna hatua iliyochukuliwa, leo napenda niweke msimamo wangu wazi katika maeneo yafuatayo;
1. Kwakuwa nilijitahidi sana kwa kila namna kujenga heshima ya kamati hii ya LAAC bila kupewa ushirikiano toka kwa wadau wote, TAMISEMI pamoja na BUNGE, naomba kutamka rasmi kuwa sina imani tena na Kamati hii kwakuwa imepoteza uhalali kuweza kuendelea kuwa kamati ya kusimamia na kudhibiti hesabu za serikali.
2. Kwa kuzingatia hoja hiyo, Ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya Kamati hii na kuipanga upya kwa maslahi ya Umma, heshima na hadhi ya Bunge letu.
3. Nikiwa mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Bunge, Na kwakuwa linayo mamlaka ya kumvua ubunge mbunge yeyote kwa azimio la Bunge, nitaiomba Kamati kushughulikia suala hili kibunge na kuhakikisha tunakwenda na azimio katika mkutano ujao wa Bunge kuhakikisha hatua stahiki zinachulikuwa kulinda heshima ya Bunge ili muhusika aendelee kuchukuliwa hatua za kijinai kama raia wa kawaida.
4. Kwakuwa suala hili linahusu heshima na hadhi ya Bunge, Ni muhimu Kamati ya Uongozi kuhakikisha suala hili linakuwa la kwanza katika ratiba za vikao vya mkutano ujao. Napenda kurudia kuwa, nilisema mwanzo na hakuna aliyechukua hatua. Hii ni mara ya mwisho na ninaahidi kutoendelea kushiriki tena vikao vya kamati hii ya aibu kama Mh. Spika hataona busara na umuhimu wa kuipangua kamati hii. Serikali legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwakuwa ni kazi ya Bunge kusimamia na kuidhibiti serikali kikatiba. Watendaji wa serikali kujua bei za wabunge ni msiba.
…………………………………………
David Kafulila (MB).
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII