HABARI MPYA LEO  

ZITTO Vs WAZIRI MKUU

By Maganga Media - Apr 22, 2012


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na wabunge, John Mnyika wa Ubungo (kushoto), Kabwe Zitto wa Kigoma Kaskazini  na Hamad Rashid wa Wawi, kwenye jengo la Utawala la Bunge Mjini Dodoma Aprili 21, 2012. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ili kuinusuru Serikali ni Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo,Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige. Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu.

Taarifa zilizopatikana juzi usiku zilieleza kuwa katika kikao hicho, mawaziri hao kwa pamoja waliwekwa katika eneo maalumu na wakawa wakiitwa mmoja mmoja kwa ajili ya mahojiano na wabunge na baadaye kupewa msimamo wa chama.

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Waziri Mkuu akaendesha kikao kingine cha faragha, safari hii kikimhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Frederick Werema na Waziri William Lukuvi. Wengine walioitwa katika kikao hicho ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mwigulu Mchemba,Katibu wa Oganaizesheni na Mahusiano ya Nje Januari Makamba na Katibu wa wabunge wa chama hicho, Jenister Mhagama.

Hata hivyo mwenye mamlaka ya kuwafukuza Mawaziri kwa mujibu wa Katiba ni Rais Jakaya Kikwete aliyewateua ingawa hata hivyo badhi ya wabunge wanamtuhumu Rais kuwa si mtu wa kufanya maamuzi haraka na kwa shinikizo.
Zitto aendelea kutafuta saini

Katika hatua nyingine,Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hoja ya kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokuwa na imani ipo pale pale kama mawaziri wanaotajwa kwa ufisadi hawatajiuzulu kufikia kesho. “Sisi tunasema bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa mawaziri waliotajwa hawatatoka na wasipotoka madudu haya yatarudia…kwa hiyo ni wao mawaziri kupima na kuwajibika au wamweke reheni Waziri Mkuu,”alisema.

Mbunge huyo alirejea wito wake wa kuwaomba wabunge wenye uchungu na ubadhirifu na ufisadi waunge mkono utiaji wa saini hizo na kwamba kama mawaziri watajiuzulu ifikapo Jumatatu, wataondoa hoja hiyo.


Kwa upande wake, Kiongozi wa Kambi rasmi ya upizania Bungeni, Freeman Mbowe alirejea msimamo wake wa kuomba kufanyiwa mabadiliko ya katiba ya nchi na kanuni za Bunge ili Spika asiwe anatokana na chama chochote cha siasa. Mbowe alitoa kauli hiyo kutokana na kile alichodai,  hatua ya Spika Anne Makinda kutafsiri vibaya kanuni za Bunge na Katiba ya nchi ili tu kuilinda Serikali na Waziri Mkuu wake ili asipigiwe kura ya kutokuwa na imani.


“Mambo ya ajabu sana eti Spika anasema hili zoezi letu ni batili…sisi tunamshangaa, wanasheria wanamshangaa na hata wananchi wanamshangaa… anatoleaje mwongozo kwa kitu ambacho hakipo mezani kwake?”alihoji.


Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kanuni inataka ili hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu iweze kufikishwa ofisi ya Spika, ni lazima ipate sahihi za wabunge 70 na ndicho wanachokifanya.

Wasomi wazungumza

Baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu wamelitaka Bunge kufuata sheria na kanuni za Bunge kabla ya kufanya maamuzi hayo kwa sababu mawaziri hao wanaripoti kwa Rais Jakaya Kikwete na si Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema kuwa, kutokana na hali hiyo wabunge hao wanapaswa kufuata kanuni ili waweze kutambua kuwa mwenye mamlaka ya kuwaondoa mawaziri hao ni  Rais na si Waziri Mkuu, hivyo basi kumlazimisha aondoke madarakani ni sawa na kumuonea.

“Mimi naona wanamuonea bure Waziri Mkuu Pinda, kwa sababu hana mamlaka ya kuwaondoa Mawaziri madarakani badala yake wanatakiwa kuangalia kanuni kwanza ndipo waweze kufanya maamuzi,”alisema Profesa Simon Mbilinyi mwasiasa mstaafu nchini.

Aliongeza kutokana  na hali hiyo wabunge hao walipaswa kumuandikia barua Rais Kikwete na kumtaarifu kuwa mawaziri wake wameshindwa kufanya kazi badala yake wanatakiwa kuwajibika kulingana na makosa waliyofanya.

Alisema kutokana na hali hiyo maamuzi ambayo yangeweza kutolewa na rais yangekuwa sahihi kwa sababu yamefuata sheria na taratibu zilizotungwa na Bunge.

Alisema kitendo cha wabunge hao kumshinikiza Waziri Mkuu kujiuzulu au kuwaondoa mawaziri hao ni kinyume na sheria na ni sawa na kumuonea, jambo ambalo linaweza kumfanya afanye maamuzi bila ya kufuata taratibu.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII