HABARI MPYA LEO  

Watu 15 watuhumiwa kuwakata mapanga Wabunge- MWANZA

By Maganga Media - Apr 4, 2012

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza, limewakamata watu 15 wanaosadikiwa kuwakata mapanga wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Salvatori Machemli wa Ukerewe. Pia jeshi hilo limesema kuwa upo ulazima wa kuwahoji wabunge hao ili polisi wapate taarifa sahihi juu ya suala hilo zito.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), amethibitisha kwamba watuhumiwa hao wamekamatwa na wameunganishwa na watu waliowavamia na kuwajeruhi baadhi ya wanawake ambao walikutwa wakijadili namna ya kwenda kusimamia kura za wagombea wao katika kata ya Kirumba jijini hapa.Polisi imesema, kazi ya kuwahoji watuhumiwa hao 15 inaendelea na kwamba lazima hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahalifu watakaobainika kutenda kosa hilo bila kuangalia chama gani na wana rangi au umbo gani.

Kamanda huyo amesisitiza kuwa upo ulazima wa kuwahoji wabunge hao ili kupata taarifa kamili kutokana na utata wa tukio hilo na kujua ni kwa nini walienda eneo hilo usiku bila kuwasiliana na polisi kwa ajili ya usalama wao. “Lakini kwa hawa waheshimiwa tutawahoji pale inapobidi kufanya hivyo. Mimi sijasema tutawakamata, inawezekana tukawahoji ili kupata maelezo yao. Na kama kuhojiwa kwa wabunge hawa si lazima polisi Mwanza, wanaweza kuhojiwa sehemu yoyote maana polisi tuko kila sehemu,” alisema Kamanda Barlow huku akikataa kuwataja majina watu hao 15 kwa madai kwamba upelelezi bado unaendelea.

Juzi, Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, Deusdedith Nsimeki (RCO), aliiambia Tanzania Daima kwamba wanatarajia kuwakamata na kuwahoji wabunge hao wanaoendelea na matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata. Katika maelezo yake, RCO alisema polisi wanaweza kuwakamata wabunge hao, wakiwa bado wamelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wanakopatiwa matibabu, au inaweza kuwasubiri watoke hospitalini kisha iwakamate.

Juzi Machemli alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akilituhumu jeshi la polisi kwa madai kwamba wakati wakishambuliwa na kuumizwa walikuwepo baadhi ya askari polisi wakiwa na SMG na kwamba alijaribu kujivuta kwenda kumshika mguu askari polisi mmoja ili amnyang’anye silaha ili ajiokoe, lakini alipigwa teke. “Aisee nimepata kipondo kama mbwa mwizi. Tumepigika hasa...lakini wakati tunashambuliwa na kukatwa mapanga walikuwepo askari polisi hatua chache wanatuangalia na SMG. Nilijivuta kumsogelea polisi nimnyang’anye silaha nijisaidie lakini akanipiga teke nikaendelea kupata kipondo,” alisema Machemli wakati alipohojiwa na mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Nchini Uingereza (BBC), Erick David Nampesya.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII