HABARI MPYA LEO  

ENGLISH YAZUA BALAA BUNGENI

By Maganga Media - Apr 18, 2012

UCHAGUZI wa wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), ulifanyika jana huku ukitawaliwa na baadhi ya vituko baada ya baadhi ya wagombea kujichanganya kujieleza kwa lugha ya Kiiingereza na wengine wakimtaja Spika kwa jina la 'Mr' badala ya 'Madam Spika'.

Wagombea walianza kujieleza mbele ya  wabunge saa 5 asubuhi na waliendelea na zoezi hilo mpaka saa 11 jioni wakati ambao kura zilipigwa na kisha bunge kuairishwa hadi saa 1 jioni kwaajili ya kutolewa majibu ya kura hizo.

Baadhi ya wagombea hao walionekana kushindwa kuelewa maswali waliyokuwa wakiulizwa na wabunge kitu kilichosababisha wengine kusema hawajui vile vilivyokuwa vikiulizwa kama vipo.

Mbali na baadhi ya wagombea hao kusuasua katika kuzungumza Kiingereza, baadhi ya wabunge nao walikuwa wakiuliza maswali kwa kusuasua kitu ambacho kilionyesha dhahiri lugha ya Kiingereza ni tatizo.

Hata hivyo kuna baadhi ya wagombea waliweza kujieleza vizuri na kueleweka na hata baadhi ya wabunge waliweza kuuliza maswali yaliyoeleweka japokuwa ujibuji wa maswali hayo ulikuwa ukienda tofauti na kile kilichoulizwa.

Wagombea waliojinadi na kuulizwa maswali na wabunge jana walikuwa ni 32, kundi namba moja likiwa na wagombea saba, kundi namba mbili wagombea tisa, kundi namba tatu wagombea sab na kundi namba nne wagombea tisa.

Wabunge waliweza kuuliza maswali 96 wagombea hao, kila mmoja akiulizwa maswali matatu na kupewa dakika 3 za kujieleza kabla ya kuulizwa maswali.

Baadhi ya wagombea walionekana kushangiliwa huku Spika akiwataka wabunge kutokufanya hivyo bali watulie kwa kuwa wabunge walitakiwa kuwasikiliza na kuwauliza maswali tu kabla ya kupiga kura.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII