"Mkapa ahusishwa na kifo cha utata cha Mwl.Nyerere"
By Maganga Media - Mar 14, 2012
Rais mstaafu wa awamu ya pili Mh B. W. Mkapa |
VITA ya maneno, vijembe na kejeli kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha imeanza.Baada ya juzi Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kufanya uzinduzi wa kampeni za CCM na kuipiga vijembe CHADEMA, chama hicho jana kilijibu mapigo kupitia kwa Mbunge wa Msoma Mjini, Vincent Nyerere, ambaye ni Naibu Meneja wa Kampeni wa CHADEMA.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni maeneo mbalimbali, mbunge huyo alishusha tuhuma nzito juu ya kile alichokiita ‘utata’ wa kifo cha Mwalimu Nyerere huku akihusisha na maamuzi ya Mkapa kung’ang’ania Mwalimu aende kutibiwa Uingereza baada ya kuanza kumkosoa juu ya sera za ubinafsishaji. Nyerere ambaye ni mmoja wa wanafamilia wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, akiwa amekulia katika familia hiyo, aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kuwa umefika wakati sasa Mkapa atoke hadharani afafanue alikuwa na nia gani kumlazimisha Mwalimu Nyerere akatibiwe Uingereza wakati mwenyewe alikuwa amekataa, akisema kuwa ugonjwa uliokuwa unamsumbua tayari ulikuwa unajulikana na daktari wake, Profesa David Mwakyusa, alikuwa tayari akimhudumia vizuri bila tatizo.
“Jana katika hotuba yake ametumia muda mwingi sana kuisema CHADEMA na akanisema mimi kwa jina moja kwa moja, sasa ‘kanibipu’ na mimi nimeamua kumpigia, tunamtaka kama anaweza arudi hapa Arumeru, aje ajibu maswali ya msingi juu ya ufisadi unaomwandama. Alianza kwa kuuza mashirika ya umma, akauza viwanda, ukienda leo miji mikubwa kama Dar es Salaam na kwingineko, vijana wengi wamegeuka kuwa waokota makopo kwa sababu hakuna ajira, viwanda viliuawa wakati wa Mkapa.
“Kwa kupitia sera yake ya ubinafsishaji akauza kila kitu, akauza viwanda, wawekezaji walionunua nao wakafanya ufisadi wamegeuza viwanda hivyo kuwa maghala ya kutunzia vitu vyao, viwanda ambavyo vingeweza kuajiri vijana Watanzania vikauzwa kiholela kwa bei ya kutupa, vingine wakajiuzia wao wenyewe. Misingi iliyowekwa na Mwalimu yote ikabomolewa badala ya wao kujenga nyumba juu ya misingi hiyo.
“Mashirika yaliyokuwa yakifanya kazi vizuri au ambayo yalihitaji usimamizi tu mzuri ili yafanye vizuri yakauzwa kiholela, yakauzwa kifisadi, tena mkumbuke alianza kwa kuuza benki. Mwalimu kuona hivyo akashtuka, akaanza kumhoji na kumkosoa hadharani juu ya sera yake hiyo, jamaa (Mkapa) kuona hivyo akaona huu sasa ni usumbufu, akaanza kumshawishi Mwalimu aende akatibiwe Uingereza, Mwalimu alikataa kabisa akisema kuwa ugonjwa unaomsumbua tayari daktari wake anamhudumia vema,” alisema Nyerere na kuongeza:
“Mwalimu alikuwa akihoji inakuwaje reli inakufa, yeye amekazana tu na ubinafsishaji, Mwalimu akahoji inakuwaje anatoza kodi kibao na kutunza pesa, kumbe Mkapa tayari alikuwa anaandaa pesa za EPA ambazo baadaye ndizo mlizisikia kupitia kashfa maarufu ya mabilioni ya EPA. Mkapa akamng’ang’ania Mwalimua akatibiwe Uingereza, akasema naye ni mmoja wa wanafamilia yetu, basi tukakubali, lakini mnajua kuwa Mwalimu alikwenda anatembea akarudi amenyamaza ndani ya jeneza?
“Sasa Mkapa atuambie ukweli juu ya hili, aje ajibu maswali yote haya, nitakuja na vigongo vingine, lazima tupambane na ufisadi hadi mwisho. Ilifikia mahali hata taarifa za ugonjwa akawa anatoa yeye Mkapa, oooh
mara Mwalimu amepatwa na mkanda wa jeshi, mara oooh leo imekuwa hivi,badala ya daktari wake. Baada ya Mwalimu kufariki dunia, wakamwambia yule daktari wake agombee ubunge watampatia uwaziri, ndivyo
ilivyotokea,” alisema Nyerere.
Aliongeza kusema kuwa pamoja na uhakika wa maisha yake baada ya kustaafu ambapo anagharimiwa kila kitu kwa kodi za Watanzania, bado Rais Mkapa alijimilikisha mgodi wa Kiwira ambao baada ya kelele nyingi za nguvu za umma, zikiongozwa na CHADEMA bungeni na nje ya Bunge,hatimaye umerudishwa kwa umma. Alimtaka Rais Mkapa kujibu tuhuma juu ya ufisadi katika ununuaji wa ndege, wakati tayari serikali ilikuwa na ndege nyingine mbili, moja ikinunuliwa wakati wa Mwalimu na ina uhakika wa kufanya kazi kwa miaka 100 iwapo ingefanyiwa matengenezo kadiri inavyotakiwa. Pia akamtaka kujibu hoja za Watanzania juu ya ufisadi wa rada, ambao hata Waingereza wanaupigia kelele, baada ya yeye na wenzake serikalini
kufanya ‘dili’ kujinufaisha wao badala ya kuongoza wananchi.
Nyerere aliongeza tuhuma kwa Mkapa akisema kuwa pia anatakiwa kujibu hoja juu ya mauaji ya Zanzibar ya mwaka 2001, ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania mbali ya serikali kuua raia wake kwa risasi, ilizalisha wakimbizi kwenda nchi za Kenya na Somalia. Akifafanua tuhuma za ufisadi dhidi ya Rais Mkapa, mbunge huyo alisema kuwa kama Mkapa anataka kueleweka mbele ya Watanzania wenye uchungu na
nchi yao, anatakiwa kujibu hoja za msingi juu ya tuhuma hizo za ufisadi zinazomwandama tangu akiwa madarakani hadi anastaafu.
Mbunge huyo ambaye alikuwa akihutubia mamia ya wakazi wa maeneo ya Lenguruki, Poli, Sing’isia na Nkoaranga, alisema kuwa rais huyo mstaafu anapaswa kuwa mmoja wa watu wa mwisho kusimama mbele za watu kwani hali inayolikabili taifa kwa sasa, ikiwamo ufisadi uliotapakaa ndani ya chama chake na serikali ya CCM, iliasisiwa tangu wakati wa utawala wake, kwa kuanzia na sera za ubinafsishaji zilizoua misingi ya
viwanda iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, mgombea wa CHADEMA Joshua Nassari, alisema kuwa amegombea kwa nia ya kubeba ‘mizigo’ ya wana wa Arumeru kwani anaitambua, hivyo yuko tayari kuibeba kwenda nayo bungeni Dodoma na katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, kuwasemea na kuiwajibisha serikali ili iwajibike kwa wananchi.
Joshua alionekana kuwagusa wananchi wa maeneo hayo pale alipokuwa akizungumzia kero za kila eneo husika, kama vile ardhi, maji, afya na elimu na namna ambavyo wanaweza kushirikiana pamoja na mbunge wao katika kuyatatua, iwapo watamchagua yeye ambaye amezaliwa na kukulia katika maeneo hayo na yuko tayari kuwatumikia akiwa anaishi katika maeneo ambayo wanaishi wao pia.
Aliwataka watu wa Meru wasidanganyike na maneno ya Mkapa kuwa atakwenda kumshauri Rais Jakaya Kikwete ashughulikie matatizo ya ardhi katika wilaya hiyo, kwani alishindwa kufanya hivyo wakati akiwa na
mamlaka ya urais, hawezi kuifanya kazi hiyo kwa sasa kwani rais ana hiari ya kukubali au kukataa ushauri wa mtu yeyote kwa mujibu wa katiba yetu mbovu.
“Kwa mujibu wa katiba yetu mbovu ambayo tunataka tuiandike upya, rais halazimiki kuchukua ushauri wa mtu yeyote, hivyo Kikwete anaweza kukataa ushauri wake huyo Mkapa, aje ajibu hoja hapa kwa nini
alishindwa kutatua matatizo ya ardhi kwa watu wa Arumeru wakati akiwa madarakani?” alihoji Nyerere.
CHANZO: Tanzania daima 14 Machi 2012
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
HABARI ZINAZOHUSIANA NA HII KATIKA news