Mwakyembe atimua vigogo ATCL
By Maganga Media - Jun 6, 2012
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ametengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Paul Chizi na amewasimamisha kazi wakurugenzi wanne kutokana na “ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, ambao umetishia uhai wa shirika hilo muhimu kwa taifa.”
Kutokana na hatua hiyo, Dk Mwakyembe amemteua rubani wa siku nyingi katika shirika hilo, Kapteni Lusajo Lazaro kukaimu nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Chizi.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Omary Chambo alisema Dar es Salaam jana kwamba Waziri amefikia uamuzi huo kutokana na taratibu za uteuzi kwa wafanyakazi wa umma kutokufuatwa.
Alisema nafasi aliyopewa Chizi haikutangazwa kama sheria na kanuni zinavyotaka... “Uteuzi wake haukufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, hivyo kupitia Sheria Na 8 ya mwaka 2002 na kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 Na 17(4), Dk Mwakyembe ametengua uteuzi huo kuanzia jana.” “Kanuni hii inaeleza bayana kuwa kama mtumishi atakuwa ameteuliwa kwa kukiuka Kifungu cha 17(1 au (3) za Kanuni za Utumishi za mwaka 2003, itakuwa ni mamlaka ya uteuzi wa kutengua uteuzi wa utumishi wake mara moja.”
Kabla ya kuteuliwa na kushika wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Chizi aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Community Airline.
Wakurugenzi wanne waliosimamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi, John Ringo, Mwanasheria wa ATCL, Amini Mziray, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Josephat Kagirwa.
Mhandisi Chambo katika taarifa yake kwa umma, alisema kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu, itaundwa kamati yenye wajumbe watatu wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria kuchunguza matumizi ya fedha zilizopokewa kuanzia mwanzoni mwa Mei mwaka huu.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII