HABARI MPYA LEO  

Mtazamo wa Mnyika juu ya mgomo wa madaktari

By Emmanuel Maganga - Jun 29, 2012


Sababu ya hali tete ya nchi na maisha ya wananchi kwenye sekta ya afya ni udhaifu wa serikali na uzembe wa bunge. Rais Jakaya Kikwete ajitokeze alitangazie taifa kuunda tume huru ya kuchunguza kutaka kuuwawa kwa Dk. Ulimboka Steven na kutoa ahadi ya kuongeza fedha katika bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kushughulikia chanzo cha mgogoro. Spika Anna Makinda aruhusu bunge litumie mamlaka yake ya kuisimamia serikali kusuluhisha.

Taifa limeingizwa kwenye hali tete katika sekta ya afya na maisha ya wananchi wanaotegemea huduma toka hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma yapo mashakani.
Tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa serikali wa kushughulikia matokeo badala ya chanzo cha mgogoro wake na madaktari na uzembe wa bunge katika kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kusuluhisha pandembili zinazolumbana kwa gharama ya vifo na nyingi kwa wagonjwa wasio na hatia.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilianza ikashindwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alijaribu akashindwa, Rais Jakaya Kikwete naye akaingilia kati kuondoa udhaifu uliokuwepo naye anaelekea kushindwa; kwa kuwa wote wanashughulikia matokeo ya mgogoro badala ya chanzo.
Chanzo cha mgogoro wa serikali na madaktari na wananchi kuhusu sekta ya afya ni bajeti finyu inayotengwa na serikali na kiasi kidogo cha fedha kinachotolewa katika sekta hii nyeti, na hivyo kushindwa kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya wakiwemo madaktari kwa upande mmoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa upande mwingine.

Rais Kikwete ajitokeze alitangazie taifa kuunda tume huru ya kuchunguza kutaka kuuwawa kwa Dk. Ulimboka na kutoa ahadi ya kuongeza fedha katika bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kushughulikia chanzo cha mgogoro:

Hatua ya serikali kukimbilia mahakamani na kutumia kivuli cha mahakama kukwepa kushughulikia madai ya msingi ya madaktari ni kuendelea kushughulikia matokeo na hivyo kuendeleza migogoro na migomo.

Hata kama serikali ikitumia vyombo vya dola kukamata au kujeruhi madaktari, inapaswa kutambua kwamba mgomo wenye madhara makubwa kwa nchi umekuwa ukiendelea chini chini kwa muda mrefu kwenye sekta ya afya nchini na kuchangia vifo vya wananchi kwa magonjwa yanayotibika kutokana na huduma mbovu na kukosekana kwa madawa na vifaa tiba katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma.

Rais Kikwete anapaswa kujitokeza na kutoa ahadi ya kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuongeza fedha za bajeti ya afya katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia mkutano wa nane wa bunge unaoendelea hivi sasa ili kushughulikia chanzo badala ya kupanua wigo wa migogoro katika taifa.
Aidha, Rais Kikwete anapaswa kutumia nguvu zake za ukuu wa nchi na uamiri jeshi mkuu kulaani tukio la kutekwa, kuteswa na kutaka kuuwawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dr. Ulimboka Stephen ambapo baadhi ya watumishi wa serikali na askari wa vyombo vya dola wanatuhumiwa kuhusika. Ili kurejesha imani juu ya Serikali na vyombo vyake badala ya kutegemea jopo la wapepelezi kutoka jeshi la polisi pekee ambalo nalo baadhi ya vituo vyake Jijini Dar es salaam vimetuhumiwa, Rais Kikwete aunde tume huru ya kuchunguza tukio husika ambalo limeongeza madoa kwa nchi kitaifa na kimataifa.

Spika aruhusu bunge litumie mamlaka yake ya kuisimamia serikali kusuluhisha:
Kwa kipindi cha takribani miezi minne nimetumia njia za kibunge kutaka suala la madai ya madaktari lijadiliwe bungeni ili kushughulikia chanzo badala ya matokeo hata hivyo hitaji hilo la kikatiba limekuwa likipuuzwa na kusababisha bunge lizembee kuchukua hatua kwa wakati kuepusha mgogoro na mgomo.

Izingatiwe kwamba katiba ya nchi ibara ya 63 (2) inatamka kwamba “Sehemu ya pili ya bunge (yaani wabunge) ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”.

Nawaomba wananchi wa Tanzania waliotutuma kuwawakilisha kumtaka Spika Makinda na wabunge wote kuwajibika kujadili bungeni hali tete ya sekta ya afya nchini na kauli tata za serikali katika kushughulikia hali hiyo. Spika, uongozi wa bunge na wabunge kwa pamoja tutakiwe kukataa visingizio vya serikali vya kutumia mahakama kuathiri haki, kinga na madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali juu ya suala la madaktari na hali ya sekta ya afya nchini.
Hivyo; wabunge, umma na wadau wa haki za binadamu tuungane pamoja kutaka Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia suala la madai ya madaktari itolewe bungeni na hadharani na bunge liruhusiwe kutumia mamlaka yake ya kuisimamia serikali kujadili taarifa hiyo na kupitisha maazimio maalum ya kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea na pia kuboresha hali ya huduma katika hospitali, vituo vya afya na zahanati inayoendelea kutetereka.

Kanuni ya 64 (1) (c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoelekeza kwamba “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika bunge, mbunge hatazungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama”; inatumiwa vibaya na serikali kuficha udhaifu na kudhibiti mamlaka ya bunge kwa kisingizio cha mahakama.

Hata hivyo, zipo njia zaidi ya nne ambazo umma unaweza kutaka spika na wabunge wazitumie kukwepa bunge kuonekana linazembea kuchukua hatua za kuisimamia serikali na kuokoa maisha ya wananchi katika hatua hii ya dharura.

Mosi, hoja inaweza kutolewa ya kutengua kanuni husika kuliwezesha bunge kujadili Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu madai ya madaktari kwa kuwa imekuwa kawaida kwa serikali kutoa hoja za kutengua kanuni wakati mwingine kuilinda serikali na kupunguza madaraka ya bunge. Mathalani, kanuni ya 94 inayolitaka bunge kukaa mwezi Februari kama Kamati ya Mipango kutoa mapendekezo ya mpango wa taifa, ilitenguliwa na matokeo yake ni kuwa serikali iliandaa bajeti ikiwemo ya sekta ya afya na kuwasilisha mwezi Juni bajeti ya serikali isiyozingatia kwa ukamilifu mpango na madai ya madaktari.

Pili, Spika anaweza kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni 114 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kutaka kamati husika ya bunge kukutana kwa dharura na kuishauri wa haraka serikali kufuta kesi iliyoko mahakama kuu kitengo cha kazi ili kulipa fursa bunge kutumia madaraka yake ya kikatiba kujadili na kupitisha maazimio ya kuweza kusuluhisha pandembili za mgogoro badala ya mahakama. Uamuzi wa kurejea mahakamani unapaswa kuwa wa mwisho baada ya hatua zingine kushindikana.

Tatu; Spika kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya 114 (17) na 116 kuitaka Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kupatiwa na kupitia nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, na kuandaa taarifa maalum ya masuala yanayoweza kujadiliwa bungeni bila kuingilia suala lililo mahakamani. Izingatiwe kwamba Serikali imefungua kesi dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na haijafungua kesi dhidi ya Jumuiya ya Madaktari na Taasisi zingine katika sekta ya afya; hivyo kufunguliwa kwa kesi hiyo hakuwezi kulizuia bunge kujadili masuala mengine yanayohusu madaktari na sekta ya afya nchini.

Nne; Kanuni ya 53 (2) au 47 (1) za Kanuni za Kudumu za bunge inaweza kutumiwa kwa Waziri husika kwamba suala la namna ambavyo serikali imejipanga kutoa huduma katika hospitali kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea au mbunge yoyote kutoa hoja kuhusu hali kwa sasa ilivyo katika hospitali na sekta ya afya kwa ujumla kufuatia kuendelea kwa mgogoro kati ya serikali na madaktari na masuala hayo yakajadiliwe. Izingatiwe masuala hayo hayahusu mgogoro ulioko mahakamani bali ni ya dharura kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi kwa wananchi na nchi kwa ujumla wakati taifa likisubiri taratibu za mahakama kukamilika.

Ni muhimu umma ukapuuza taarifa isiyokuwa ya kweli iliyotolewa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni tarehe 27 Juni 2012 ya kudai kwa tayari kamati ya huduma za jamii imewasilisha taarifa yake bungeni wakati ambapo taarifa hiyo iliyohusisha kazi ya kubwa ya kamati na matumizi ya ziada ya fedha za wananchi imefanywa kuwa siri hata kwetu wabunge. Naibu Spika Ndugai kwa kauli hiyo amekwepa kutekeleza muongozo wake mwenyewe alioutoa katika mkutano wa sita wa bunge mwezi Februari mwaka 2012 kwamba baada ya kamati kumaliza kazi yake taarifa ingewasilishwa bungeni na kujadiliwa. Tayari nilishamuandikia barua Spika tarehe 27 Juni 2012 kupuuza maelezo hayo ya Naibu Spika na kutoa kwa wabunge na bunge taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii ili wabunge tusiendelee kupokea kauli za upande mmoja wa serikali bila kuwa na maelezo na vielezo vya upande wa pili wa madaktari.
John Mnyika (Mb)Bungeni-Dodoma
28/06/2012

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII