HABARI MPYA LEO  

Kesi ya Lulu bado!

By Maganga Media - Jun 5, 2012


UPELELEZI wa kesi ya mauaji inayomkabili muigizaji nyota wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu bado haujakamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Jana Wakili wa Serikali, Peter Sekwao aliieleza mahakaama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo na hadi Juni 18, 2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alilazimika kupandishwa kizimbani mara mbili baada ya tarehe ya kutajwa tena kukosewa. Awali, hakimu Mmbando alisema kuwa kesi hiyo ingetajwa tena Juni 28 kisha mshtakiwa huyo akaondolewa mahakamani na kupelekwa mahabusu akisubiri kurejeshwa mahabusu ya gereza la Segerea.Baadaye alirudishwa tena mahakamani na kupandishwa kizimbani baada ya kubainika kuwa tarehe iliyopangwa ya kutajwa kwa kesi hiyo haikuwa sahihi kwani karani alikuwa amekosea kuhesababu, ndipo ikapangwa Juni 18.

Jalada hilo lilipelekwa Mahakama Kuu Ijumaa ya Mei 18, mwaka huu baada ya jopo la Mawakili wa mshtakiwa  huyo kuwasilisha maombi juu ya uchunguzi kuhusiana na umri halali wa msanii huyo. Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata kama ni mtoto au ni mtu mzima, jambo ambalo limewalazimu mawakili hao kuwasilisha maombi hayo ya uchunguzi wa umri wake Mahakama Kuu.Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili Peter Kibatala Mei 15, 2012 na yamepangwa kusikilizwa  na Jaji Dk Fauz Twaib Mei 28, 2012.

Akifafanua juu ya maombi hayo Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) alisema kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa.

Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  ili mahakama iweze kujiridhisha kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kujipa angalizo juu ya maslahi ya mtoto. “Baada ya uchunguzi huo mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria hiyo ya mtoto,” alisema Wakili Kibatala.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII